Sunday, February 19, 2012

Mjue bibi Cheka mwanamuziki mzee wa Bongo Fleva

     
 Katika  kukuwa kwa muziki wa kizazi kipya maarufu kama Bongo Fleva , kumepelekea kuibuka kwa wasanii wapya wadogo kwa wakubwa, na kufanya muziki huo kuwa na taswira tofauti. Hivi karibuni kwenye tasnia hiyo kumeibuka  msanii mpya,  Cheka Hija ‘Bibi Cheka’  ambaye  ameweka rekodi kwa kuwa msanii mwenye umri mkubwa kuingia kwenye tasnia hiyo kuliko wote hapa Tanzania.

Mwanamuziki huyo  alielezea sababu zilizomfanya aingie kwenye muziki huo, ambao ulikuwa kichwani mwake kwa muda mrefu. Alianza kwa kusema kwamba aliingia kwenye tasnia ya muziki mwaka 1978 akiwa na umri wa miaka 12, wakati huo alikuwa akiishi na mama yake Asha ambaye alikuwa ametengana na mumewe mzee Hija.
Bi Cheka anasema nyumba yao ilikuwa  maeneo ya Kariakoo mtaa wa Kriki kabla ya kubadilishwa jina na kuitwa mtaa wa Lindi.Kwakuwa alikuwa mtundu sana na mkorofi hivyo alivutiwa sana na muziki, hali iliyompelekea akijifunza jinsi ya kucheza kupitia kwenye bendi mbalimbali zilizokuwa zikipiga kwenye mabaa na mahoteli.
Alijifunza sana kucheza muziki kutoka kwa watu wa jamuhuri ya Demokrasia ya Kongo, bendi za ndani ya nchi na ngoma za asili. “Niliifanikiwa kuzijua haraka kwakuwa nilikuwa mwepesi sana katika kucheza, pia muziki nilikuwa naupenda” alisema Bi Cheka. Baada ya kujifunza kwa muda mrefu, ndipo alipoamua kuanza safari ya  kwenda Ilala walipokuwa wakifanya mazoezi bendi ya Msondo Ngoma ‘Baba ya Muziki’. Alisema wakati bendi ya Msondo Ngoma ikifanya mazoezi, naye pia alikuwa akiutumia muda huo kwa kucheza. Hali hiyo ilimpekea kuunda  kundi la watu 16, ambao walikuwa wanachama wa bendi hiyo katika upande wa Unenguaji.
Kwakuwa alikuwa na uzoefu katika unenguaji hivyo ikambidi, awafunze  wenzake, jinsi ya kucheza ngoma mbalimbali kiasi cha kumwita Kocha. Cheka alisema kwakuwa umri wake ulikuwa mdogo,  miaka 14 hivyo mzee Muhidin Gurumo ndiye aliyekuwa akifika kwao na kumuombe ruhusa kwa mama yake ilikwenda kucheza kwenye bendi pindi linapokuwepo onyeasho.
Aidha bi Cheka anasema ingawa alikuwa akijitolea sana katika suala la uchezaji lakini kwa kipindi hicho kulikuwa hakuna kulipwa, zaidi ya kuambulia umaarufu na kufanya kama vile hobi.
Hata hivyo anasema muziki ukaanza kumfanya ajue mikoa mbalimbali, kwani safari yake ya kwanza alikwenda Mbeya, ambapo wakaenda hadi Bukoba na baada ye kupitia Morogoro na baadaye kurudi Dar es slaam na huko kote alikuwa na kazi moja ya kuonyesha uwezo wake wa kucheza. Anasema kitu ambacho anakikumbuka sana ni lile shindano alilofanya mkoani Morogoro, lililoitwa Shingari, likiusisha bendi ya Moro Jazz na Msondo Ngoma.
Yeye alipanda jukwaani akiwa na Damas Damson na Mguno Mambeta ambaye alikuwa kaka yake na mwanasoka wa Simba Hassan Mambeta. Bi Cheka alisema siku hiyo alijitahidi kucheza kadri ya uwezo wake, na hatmaye waliibuka washindi na kutunikiwa vifaa vya muziki. Kutokana na ujuzi aliouonyesha pale jukwaani ndipo akaanza kutafutwa na wanaume, jambo ambalo lilimfanya Gurumo amchukue na kwenda kumficha ndani ya gari. Aliweza kufichwa humo  hadi asubuhi huku akishudia wenzake wakiondoka na wanaume na wengine wakiondoka na wanawake, lakini yeye umri wake ulikuwa haukumruhusu kufanya hivyo.
Mwaka 1973 aliweza kupata mtoto wake wa kwanza akiwa na Juma Fundi, ambaye alikuwa kama mpenzi wake.  Alisema kwa kipindi hicho alikuwa akifanya muziki, pindi anapopendana  na mtu basi alikuwa radhi wakubalianae lakini alikuwa akihofia kukimbia na fedha za mtu kama walivyokuwa wakifanya wengine.
Bi Cheka aalisema kwamba alikuwa na kipaji na sauti ya kuimba, na hili lilikuja kujidhihilisha, pindi alipokuja Hamisi Franswa ‘Mfaransa’ na kumuimbisha kifaransa, na kukikariri chote na hatmaye akaja kuimba kwenye hoteli. Alisema ilipofika mwaka 1988 ndipo akaamua kuachana na muziki, baada ya kuona haulipi na umri tayari ulikuwa umeshaanza kusogea wakati majukumu nayo yakiongezeka, ndipo akaanza maisha mapya  maeneo ya Bunju. Huko aliweza kujiingiza kwenye uvunjaji wa mawe’Kokoto’ na kuuza kwa watu wenye magari, wakati huo akiendelea uhusiano wake na Juma Fundi ambaye baadaye alikuja kuzaa naye watoto  watano.
Mtoto wakwanza alimzaa 1973 ambaye ni Nacho wakafuata  Siwa, Fatuma, Adam na wa mwisho ni Kombo aliyemzaa 1983.  Alisema maisha yalianza kubadilika baada ya kuachika na mumewe ambaye aliishi naye kwenye uchumba miaka 12, na walipofunga naye ndoa alimwacha baada ya kutimiza mwaka mmoja na nusu.
Pigo lingine ambalo lilimchanganya pindi alipopata msiba wa watoto wake, ambao ndiyo walikuwa wakimsaidia Nacho Juma Fundi na Siwa Juma Fundi na ndipo alipoona maisha magumu hadi kutamani kufa.  Anasema hata hivi alikuja kuachana na kazi hiyo ya uvunjaji wa makokoto, mwaka 1994  kutokana na bosi mmoja ambaye walikuwa wakimfanyia kazi kuondoka na fedha na kuliacha deni ambaye yeye ilimbidi alilipe.
Lililikuwa deni la gari 16 ambazo yalihitaji kujazwa kokoto, jambo ambalo alishirikiana na wenzake katika kulipa lakini yeye ilibidi pia kuwalipa na hao waliokuwa wakimsaidia. Anasema deni hilo lilimtesa sana, na hivyo baada ya kumaliza, aliamua kuachana na kazi hiyo baada ya hapo akarudi nyumbani na kuanza kupika maandazi kwaajili ya biashara.
Mambo pia hayakumwendea vizuri kwani ilipofikia mwaka 1999 aliungua na mafuta ya kula aliyokuwa akikaangia maandazi, wakati akijaribu kuyaepua  kwenye jiko na kumwachia kidogonda kikubwa. Baada ya kuugua na mafuta ya kupikia, alishindwa kuendelea na upikaji wa maandazi na kuanza biashara nyingine ya ushona wa mashuka ya kutandikia maarufu kama mashuka ya Kigoma, kazi anayoifanya mpaka leo.  Mwaka 2006  ndipo akavutiwa na  kijana Peter ‘P Star’ni jilani yake ambaye ni msanii wa Bongo fleva.  Alivutiwa sana kutokana na uwezo bado alikuwa nao, ikabidi kujiunga na huyo kijana na vijana wengine, katika kuwafundisha jinsi ya kuandika mistari na kuimba.
“Niliweza kumwelekeza jinsi ya kuimba na hata kumsaidia kutunga na nyimbo zingine kumtungia” alisema bibi.  Anasema nyimbo ambazo alimtungia huyo kijana huyo ziliweza kwenda studio na kurekodiwa, lakini hazikuweza kufanya vizuri. “Hapo sasa ndipo nikaanza kufikiria ni jinsi gani niweze kufika kwa Saidi Fella na kumueleza lengo langu” alisema.  
Bi Cheka alisema ndipo akaanza kupanga mikakati kwa kumuomba  kijana  huyo kumfikisha kwenye maskani ya Saidi Fella ya maarufu kama  maskani ya Mkubwa na Wanawe.  Anasema alipofika kwa Fella akatambaulishwa kwa Temba, ili aweze kuongea naye na hapo ndipo alipoanza kuimba nyimbo zake nyingi na hatmaye kuchaguliwa moja ya NI wewe.
Nyimbo hiyo akaanza kuifanyia mazoezi katika studio ya Poteza Record, iliyotengeneza wimbo wa  Naenda kusema wa Aslay Sadiq ‘Dogo Aslay’, chini ya mtayarishaji Suresh ‘Mr India’. Anasema baada ya hapo wimbo uliisha na hivi sasa yupo kwenye mikakati ya wisho katika kumalizia video ya wimbo huo, akiwa amemshirikisha Temba.
Huyo ndiyo Bibi Cheka, ambaye amezaliwa 1960 Dar es salaam, na kusoma dalasa la nne la mkoloni. Alisema shule ya awali alisoma Zanzibar kwa babu yake mzaa baba na kuja kumalizia shule ya wanawake ya jijini Dar es salaam. Kwa kabila yeye mwenyewe anajiita mzalamo lakini kiulkweli kwa baba ni Msanga na mama ni Mluguru.
Mwisho



No comments:

Post a Comment

https://www.facebook.com/gomesamohamedi