SERIKALI kupitia wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo imewakatia bima ya mwaka mmoja wasanii walioshinda Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) ili kuwasaidi wanapopata matatizo.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, wakati wa ukataji wa bima hiyo , kaimu katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa Taifa (BASATA), Mniko Matiko alisema bima walizokatiwa ni bima ya Maisha katika Mfuko wa Hifadhi wa Kijamii wa NSSF.
Lakini pia wamekatiwa bima katika mfumo wa Afya wa kijamii (NHIF), ambapo baada ya mwaka mmoja wataanza kulipia Sh 20,000 kwa mwezi.
Alisema Serikali imewalipia huduma hizo, ili kuwajengea maisha ya sasa na baadaye kutokana na wengi wao kutojiunga na mifuko hiyo kwaajili ya maisha yao ya uzeeni au wanapopata matatizo ya kiafya.
“Serikali yetu itatoa zawadi nyingi kwa washindi wa tuzo hizo, mwaka mzima tutakuwa tukifanya jambo ilimradi tuwe na kitu cha kufanya” alisema.
Jumla ya wasanii ambao walishinda tuzo hiyo ni 51 ambapo kati yao wasanii wanne wametunukiwa tuzo ya heshima na wengine wamepigiwa kura.
Mniko alisema katika kuboresha tuzo hizo kwa mwakani, wanatarajia kufanya vikao na wasanii ambao walishinda tuzo hizo ili kupata maoni yao ambayo wanaona yanafaa.
Aliongeza kwa kusema wanatarajia pia kukaa na wasanii walioshiriki lakini hawakushinda na wasanii ambao hawakushiriki kabisa ili kutoa maoni yao ili kuboresha zaidi.
Tayari kuna baadhi ya wasanii wameshaonesha nia ya wazi ya kutamani kushinda tuzo za mwakani, kwa kusema wanajiandaa na kazi nzuri ili kushindana.
Mwisho
No comments:
Post a Comment
https://www.facebook.com/gomesamohamedi