Wakati machafuko yanaendelea kutokea katuika chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) juu ya
waraka halisi wa ‘Mkakati wa Mabadiliko 2013’ uliosababisha Zitto Kabwe
kuvuliwa wadhifa wake wa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema na kikao cha Kamati Kuu
ya chama hicho kilichofanyika Novemba 20 - 22, mwaka huu.
Baada ya juzi, Mkurugenzi wa Habari
na Uenezi wa Chadema, John Mnyika kuwaeleza wanahabari kuwa waraka
uliochapishwa katika magazeti na mitandao ya kijamii, siyo halisi, aliyekuwa
Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba amejitokeza na kuutetea huku akidai kwamba huo unaodaiwa na uongozi kuwa ndiyo
halisi umeghushiwa.
Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma
Kaskazini (Chadema), alivuliwa uongozi pamoja na aliyekuwa Mjumbe wa Kamati
Kuu, Dk Kitila Mkumbo na Mwigamba kutokana na madai ya kuandaa waraka huo ambao
Chadema kimesema ulikuwa unaeleza mbinu za uasi za viongozi hao ambazo
zingetumika wakati wa uchaguzi mkuu wa ndani wa chama hicho jambo ambalo ni
kinyume na katiba, sheria na itifaki zake.
Mwigamba alidai kwamba
Kuna njama zinazofanywa na baadhi ya
viongozi wa Chadema ili kuubadili waraka halisi wa ‘Mkakati wa Mabadiliko 2013’
kwa lengo la kupoteza maana yake, huku akisisitiza kuwa waraka halisi hauna
tatizo lolote.
Katika madai yake, Mnyika alisema
waraka huo unaosambazwa na kuchapishwa, si ule uliowasilishwa na kujadiliwa
katika kikao cha Kamati Kuu na kuahidi kuutoa waraka halisi ambao una mambo
makubwa na mengi zaidi.
“Waraka utakaotumika katika
mashtaka yao siyo huo. Sisi tutautumia ule ambao uliwasilishwa katika Kamati
Kuu ambao una mambo makubwa na mengi zaidi kuliko huo unaochapishwa sehemu
mbalimbali, ikibidi tutautoa huo waraka halisi,” alisema.
Hata hivyo, jana Mwigamba alisema
waraka halisi ni ule ambao upo katika kompyuta mpakato (Laptop)
aliyonyang’anywa na wanachama wa Chadema, Oktoba 25, mwaka huu, katika mkutano
mjini Arusha.
“Waraka uliosambazwa kwenye
vyombo mbalimbali vya habari na mitandao ya kijamii ni sahihi neno kwa neno
kama nilivyousoma katika magazeti ya jana (juzi), pamoja na nakala iliyopo
katika mtandao wa kijamii wa Jamii Forums.”
Aliongeza: “Ili kuthibitisha kwamba
waraka ule ndiyo wenyewe, nawatumieni ‘soft copy’ kutoka kwenye kompyuta yangu
kwani waraka huo uliibwa kutoka katika kompyuta hiyo ambayo nilirudishiwa baada
ya wao kuikagua na kukuta waraka huo halisi.”
Mwigamba alisema waraka wake
unatofautiana kwa kiasi kikubwa na ule ambao Chadema kinasema kuwa ndiyo
halisi: “Lissu na wenzake wana mpango wa
kuuchakachua waraka huu, lakini wamekwama.”
Alisema kuandaa
waraka huo siyo uhaini kama ambavyo imekuwa ikielezwa na viongozi wa Chadema na
kusisitiza kuwa ni waraka wa kusaka ushindi katika uchaguzi halali ndani ya
chama hicho uliopangwa kufanyika Desemba mwaka huu na baadaye kusogezwa hadi
Juni mwakani.

No comments:
Post a Comment
https://www.facebook.com/gomesamohamedi