KAMPUNI I-View
Studios ya mjini Dar es Salaam imeshinda mchakato wa kurekodi video mpya ya
msanii Naseeb Abdul ‘Diamond Platnumz’ ambayo usaili wake utafanyika Jumamosi
kwenye ukumbi wa Nyumbani Lounge, Dar es Salaam.
Akizungumza
mjini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Kampuni ya One Touch Solutions, Petter
Mwendapole alisema I-View imepata nafasi hiyo kutokana na kiwango kikubwa cha
video kadhaa ilizofanya lakini pia vifaa ilivyo navyo na uwezo wa wafanyakazi
wake.
“Siku zote kila
mtu anaangalia kitu kizuri, Diamond ametaka kufanya mapinduzi katika tasnia ya
muziki, lakini kufanya mapinduzi kunahusisha vitu vingi, tungo zake yeye kama
msanii, studio anayorekodia watu watakaoshiriki kwenye video yake kampuni
itakayorekodi video pia, lakini mwisho wa siku I-View chini ya Raqey Mohamed
ndio imeshinda nafasi hiyo.
“Raqey
anafahamika kwa kazi zake pamoja na kurekodi matangazo mbalimbali ya
Televisheni, picha mnato lakini pia video za wasanii Taznim ya Kwasakwasa,
Utanikumbuka ya Suma Lee ni baadhi ya kazi ambazo zinaonyesha uwezo alionao
lakini pia Diamond na timu yake tumeweza kuona vifaa vipya na vya kisasa
ambavyo Raqey anavyo kwa sasa na hakuna kwa Afrika Mashariki na Kati,” alisema.
Kwa upande wake
Raqey ambaye ni Mkurugenzi wa I-View alisema anahitaji kuifanya kazi hiyo kuwa
tofauti ili kusukuma mbele sekta ya mawasiliano na muziki kwa ujumla.
“Sisi kama
I-View tunafurahi kufanya kazi na Diamond, ni msanii mzuri na mkubwa ambaye
kazi zake zinaonekana, hatutamuangusha na mashabiki na wasanii wengine
wasubirie kazi itakapotoka,” alisema.
I-View pia
watashiriki katika mchakato wa kupata watu watakaonekana kwenye video hiyo
ambayo ni kwa mara ya kwanza nchini kutafanywa usaili wa washiriki. Usaili huo
utafanyika Jumamosi katika ukumbi wa Nyumbani Lounge ambao unamilikiwa na
mwanamuziki Lady Jaydee. Majina ya majaji wataochuja yatanatarajiwa kutangazwa
leo.

No comments:
Post a Comment
https://www.facebook.com/gomesamohamedi